Jumapili 1 Novemba 2026 - 21:43
Kujitoa katika Mkataba wa NPT Liwe Dai la Umma katika Mikusanyiko ya Usiku/ Mlango-Bahari wa Hormuz ni Ufunguo wa Uchumi wa Dunia

Mjumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuangaliwa upya uanachama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), akisema kuwa; Iran katika kipindi cha takribani miongo mitatu ya kuendelea kuuheshimu mkataba huo, haikunufaika na manufaa yaliyoahidiwa, bali imepata hasara na madhara makubwa. Kwa msingi huo, amesisitiza kuwa dai la kujitoa katika mkataba huo linapaswa kuwa miongoni mwa matakwa ya jumla ya wananchi katika mikusanyiko ya usiku.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Mohsen Araaki amesema hayo leo asubuhi, mwanzoni mwa darsa yake ya juu ya fiqhi, alipokuwa akizungumzia umuhimu wa kuibua matakwa ya kimkakati na kitaifa katika mikusanyiko ya wananchi inayofanyika nyakati za usiku.

Amesema: "Leo, mojawapo ya matakwa muhimu yanayopaswa kuibuliwa katika mikusanyiko hii na katika maeneo yote ya nchi ni kuwaomba viongozi wapitie upya suala la kuendelea uanachama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia."

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza nchini Iran, ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika miaka iliyopita, imekumbwa na madhara na mapigo mengi kutokana na uanachama wake na kuendelea kuuheshimu mkataba huo, ilhali haikupata manufaa yoyote yanayolingana na uanachama huo. Kwa hiyo, ni muhimu viongozi, kwa kuzingatia uzoefu uliopatikana, wafanye mapitio kuhusu nchi kuendelea katika mkataba huo.

Ahadi ya kunufaika na teknolojia ya nyuklia kwa masharti ya kujiunga na mkataba haikutekelezwa

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu amesema, akizungumzia ahadi zilizokuwa zikitolewa mwanzoni mwa kujiunga Iran na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia: "Tangu mwanzoni, ilikuwa ikielezwa kuwa iwapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itajiunga na mkataba huu na kujifunga kutokwenda katika mwelekeo wa kutengeneza silaha za nyuklia, nchi wanachama na taasisi za kimataifa zitatoa vifaa na misaada inayohitajika kwa nchi hiyo, na Iran itapewa fursa na marupurupu maalumu katika eneo la kuendeleza sekta ya nyuklia."

Mjumbe wa Baraza la Kutambua Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu ameendelea kusema kuwa; kwa msingi huo, ilitarajiwa kuwa uanachama katika mkataba huu ungekuwa njia ya kuiwezesha Iran kunufaika na ushirikiano wa kimataifa, misaada ya kiufundi na vifaa vinavyohusiana na sekta ya nyuklia. Hata hivyo, sasa baada ya kupita takribani miongo mitatu tangu kuendelea kwa uanachama huo, ni lazima kuchunguza ni kwa kiwango gani ahadi hizo zimetekelezwa na zimeiletea nchi mafanikio gani.

Ayatullah Araaki amesisitiza kuwa; uzoefu wa miaka hii umeonesha kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sio kwamba haikupata tu misaada iliyotarajiwa, bali taasisi na jumuiya ambazo, kwa mujibu wa wajibu wao wa kimataifa, zinapaswa kusimamia utekelezaji wa majukumu na kutoa msaada kwa nchi wanachama wa mkataba huo, mara nyingi badala ya kuisaidia Iran, zimekuwa chanzo cha kuwekewa shinikizo na kuipatia nchi hiyo madhara.

Taasisi za kimataifa badala ya kuisaidia Iran, zilikabidhi taarifa za nyuklia za nchi hiyo kwa maadui

Mjumbe wa Baraza la Kutambua Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu, akizungumzia mwenendo wa taasisi za kimataifa kuhusiana na shughuli za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa; taasisi hizo sio kwamba hazikuilinda haki ya Iran tu, bali kupitia hatua zake ziliisababishia nchi hiyo mapigo makubwa.

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu amefafanua suala hilo kwa kusema: "Suala la kwanza lilikuwa ni ukusanyaji wa taarifa na kufanyika ukaguzi, ambao hatimaye ulisababisha taarifa nyeti za nchi hii kukabidhiwa kwa maadui.

Kwa upande mwingine, taasisi hizi, kwa visingizio mbalimbali, zilifuatilia mchakato wa kupitishwa maazimio ya kuilaani Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuweka mazingira ya kuongezeka vikwazo na shinikizo la kimataifa dhidi yake."

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza ameongeza kuwa; mwenendo huo hatimaye ulifikia hatua ambayo hata mitambo ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilishambuliwa na kulipuliwa kwa mabomu. Hali hii ilitokea wakati ambapo ilitarajiwa kuwa uanachama wa Iran katika mkataba huo na ushirikiano wake na taasisi za kimataifa vingehakikisha, angalau, nchi hiyo inapata ulinzi unaohitajika dhidi ya vitendo hivyo vya uchokozi.

Ayatullah Araaki, akizungumzia kauli za upande wa pili kuhusu kiwango cha uharibifu uliosababishwa katika mitambo ya nyuklia ya Iran, amesema: "Ni wao wenyewe wanaodai kuwa wameishambulia mitambo ya nyuklia ya Iran kwa mabomu kiasi kwamba hakuna chochote kilichobaki. Ikiwa, kwa mujibu wa madai yao wenyewe, hakuna chochote kilichobaki katika mitambo hiyo, basi swali linalojitokeza ni: Iran kuendelea kubaki katika Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia kuna uhalali gani, na kutakuwa na mafanikio gani kwa nchi?"

Mjumbe wa Baraza la Kutambua Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu amesisitiza kuwa; pale ambapo kuendelea kuwa mwanachama wa mkataba fulani hakujatekeleza tu manufaa yaliyotarajiwa, bali pia kumekuwa sababu ya kuisababishia nchi hasara kubwa, ni lazima kufanya uamuzi kuhusu umuhimu wa kuendelea kuwa mwanachama wake kwa mtazamo unaozingatia uhalisia.

Mkanganyiko katika mwenendo wa nchi za Magharibi kuhusu Iran na utawala wa Kizayuni

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu, akiendelea na mazungumzo yake kuhusu mwenendo wa pande mbili wa nchi za Magharibi katika suala la shughuli za nyuklia za Iran na utawala wa Kizayuni, ameeleza kumbukumbu ya mahojiano moja ya viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza.

Amesema: "Mimi mwenyewe, katika siku ambazo shinikizo la kufanya ukaguzi katika vituo vya nyuklia vya Iran lilikuwa limeongezeka, nilisikiliza mahojiano ya mmoja wa viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza, ambapo mwandishi mmoja wa habari aliuliza swali muhimu kuhusu mwenendo wa pande mbili wa nchi hiyo."

Mwalimu wa masomo ya juu katika Hawza ya Qum ameendelea kusema kuwa; mwandishi huyo wa habari alimuuliza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza kues: "Kwa nini mnaishinikiza sana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na, kwa kisingizio cha kutotekeleza majukumu yake ya nyuklia, mnaichukulia misimamo ya uhasama na kuiwekea vikwazo mbalimbali, ilhali utawala wa Kizayuni una silaha za nyuklia, lakini hamchukui hatua yoyote dhidi yake? Isitoshe, utawala huu kimsingi si mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia."

Ayatullah Araaki ameongeza kuwa mwandishi huyo wa habari pia alieleza kwamba Iran ni mwanachama wa mkataba huo, imeshirikiana na taasisi husika katika suala la ukaguzi wa vituo vyake vya nyuklia na imeruhusu vituo hivyo kukaguliwa. Kwa hiyo, kwa nini shinikizo za aina hiyo ziwekwe dhidi ya Iran, ilhali mnakaa kimya mbele ya utawala wa Kizayuni ambao haupo ndani ya mkataba huo na una silaha za nyuklia?

Akizungumzia jibu la Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Ayatullah Araaki amesema: "Jibu lake lilikuwa kwamba tunaiwekea Iran shinikizo kwa sababu ni mwanachama wa mkataba huu, imeutia saini na inapaswa kutekeleza majukumu yake; ilhali utawala wa Kizayuni si mwanachama wa mkataba huu."

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu ameeleza kuwa jibu hilo la wazi ni mfano bayana wa mkanganyiko na mantiki ya pande mbili unaoonekana katika mwenendo wa baadhi ya nchi za Magharibi. Maana yake ni kwamba uanachama na kukubali majukumu ya kimataifa kwa nchi kama Iran hugeuzwa kuwa chombo cha kuiwekea shinikizo, lakini mbele ya utawala ambao haupo ndani ya mkataba huo na una uwezo wa nyuklia, hatua kama hizo hazichukuliwi.

Kuendelea kuwa mwanachama wa mkataba ambao haujailetea nchi mafanikio kunahitaji kupitiwa upya

Ayatullah Araaki, akiuliza iwapo, kwa kuzingatia uzoefu wa aina hiyo, kuendelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia kuna mantiki na uhalali wa kutosha, amesema: "Leo, kwa kweli, tunapaswa kujiuliza: Je, akili na mantiki vinakubali kwamba tuendelee kubaki katika mkataba ambao haujailetea nchi manufaa yoyote, bali umelisababishia taifa la Iran hasara kubwa?"

Ameongeza kuwa; yaliyotokea katika kipindi chote cha miaka hii yanaonesha kwamba kuendelea kubaki katika mkataba huo bila kupata manufaa na misaada iliyotazamiwa kunaweza kuwa na madhara kwa wananchi na maslahi ya kitaifa ya nchi. Kwa hiyo, ni muhimu viongozi wafanye uchunguzi wa kina kuhusu uzoefu wa huko nyuma na hali ya sasa, kisha wafanye uamuzi na mapitio kuhusu kuendelea uanachama wa Iran katika mkataba huo.

Dai la kujitoa katika Mkataba wa NPT linapaswa kuibuliwa katika mikusanyiko ya usiku

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu, akisisitiza umuhimu wa kugeuza suala hili kuwa dai la jumla la wananchi, amesema: "Matumaini yetu ni kwamba mikusanyiko ya wananchi inayofanyika nyakati za usiku katika kila eneo la nchi, iweke pia dai hili katika ajenda zake na kuwaomba viongozi wapitie kuhusu kuendelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia."

Amesisitiza kuwa dai la kujitoa katika mkataba huu linapaswa kugeuka kuwa hitaji la jumla la wananchi, kwa sababu sababu ya ombi hili iko wazi: Kuendelea Iran kuwa mwanachama wa mkataba huu, kwa kuzingatia uzoefu wa miaka iliyopita, kumeisababishia nchi hasara kubwa, lakini kwa upande mwingine, hakujaliletea taifa la Iran manufaa yoyote yenye uzito.

Ayatullah Araaki ameeleza kuwa; wananchi wanapaswa kulidai suala hili kwa uzito kutoka kwa serikali na viongozi wao katika mikusanyiko yao ya usiku, ili kufanyike mapitio kuhusu kuendelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia.

Viongozi na wapiganaji wasirudi nyuma katika suala la Mlango-Bahari wa Hormuz

Ayatullah Mohsen Araaki, akizungumzia nafasi ya kimkakati ya Mlango-Bahari wa Hormuz katika mizani ya kiuchumi na kisiasa duniani, amesema: "Leo, ufunguo wa uchumi wa dunia uko mikononi mwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wapiganaji wetu, na ufunguo huo ni Mlango-Bahari wa Hormuz. Huu ndio uwezo ambao nchi nyingi zilikuwa zikautafuta ili kutatua matatizo yao, lakini sasa umuhimu na nafasi yake vimekuwa wazi."

Ameongeza kuwa leo Mlango-Bahari wa Hormuz umegeuka kuwa mojawapo ya nyenzo muhimu zaidi za kimkakati katika mizani ya kimataifa, na unaweza kutekeleza nafasi yenye maamuzi katika kutatua masuala na matatizo ambayo yamedumu kwa miaka mingi katika uwanja wa kimataifa.

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu, akisisitiza umuhimu wa viongozi wa serikali na wapiganaji kuratibu misimamo yao kwa kuzingatia mwongozo wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesema: "Matumaini yetu kutoka kwa viongozi wa nchi na wapiganaji ni kwamba, kwa kufuata kikamilifu amri na mwongozo wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, wasilegeze msimamo wao hata kidogo katika suala la Mlango-Bahari wa Hormuz."

Ayatullah Araaki, akizungumzia msisitizo wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu suala hili, amesisitiza: "Kama alivyosisitiza katika moja ya jumbe zake, Mlango-Bahari wa Hormuz haupaswi kufunguliwa tena mpaka matakwa na madai yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yatimizwe kikamilifu, bila kupunguzwa hata kidogo."

Ameendelea kusema kuwa inawezekana hata kwenda mbali zaidi ya matakwa yaliyotolewa hapo awali, kwa sababu upande wa pili kwa sasa unakabiliwa na vikwazo na shinikizo zaidi. Hapo awali, kulikuwa na matakwa saba yaliyowasilishwa katika makubaliano na mazungumzo, lakini sasa, kwa kuzingatia hali mpya, kuongezeka kwa shinikizo za kiuchumi na kupanda bei ya mafuta, upande wa pili utalazimika hatua kwa hatua kufikia hatua ya kukubali matakwa mengi zaidi.

Viongozi wasishawishiwe na propaganda na shinikizo

Mjumbe wa Baraza la Kutambua Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu, akitoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kuanzishwa propaganda za vyombo vya habari na shinikizo za ndani kuhusiana na suala la Mlango-Bahari wa Hormuz, amesema: "Viongozi wa nchi wanapaswa kuwa waangalifu wasije wakaathiriwa na shinikizo na propaganda zinazozushwa ndani ya nchi. Hii ni kwa sababu huenda, kutokana na kuendelea vikwazo vinavyosababishwa na kufungwa Mlango Hormuz na kujitokeza kwa matatizo ya kiuchumi, baadhi ya makundi yakatumia suala hilo kuwawekea viongozi shinikizo."

Ameongeza kuwa; huenda baadhi ya watu wakaibua masuala kama vile haki za binadamu na majukumu ya kimataifa, kisha wakauliza kwa nini wananchi duniani wanapaswa kukabiliwa na kupanda kwa bei na matatizo ya kiuchumi.

Kwa mfano, huenda wakazungumzia ugumu wa maisha ya wananchi wa nchi za Ulaya na Marekani kwa kurejelea kupanda bei ya vyakula katika nchi hizo, na kujaribu kutumia suala hilo kushawishi fikra za umma.

Ayatullah Araaki ameeleza kuwa kuna uwezekano wa makundi ambayo siku zote yamekuwa yakisisitiza umuhimu wa kujisalimisha mbele ya matakwa ya upande wa pili kujaribu, katika siku zijazo, kutumia vyombo vya habari kuanzisha mazingira ya aina hiyo na kujaribu kuwawekea viongozi wa nchi shinikizo ili warudi nyuma katika misimamo yao. Kwa hiyo, ni lazima kuwa macho mbele ya propaganda hizo.

Matakwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamefungamana na suala la Palestina na kusitishwa kuunga mkono utawala wa Kizayuni

Akizungumzia historia ndefu ya vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Araaki amesema: "Taifa la Iran limekuwa likikabiliwa na vikwazo na shinikizo mbalimbali kwa kipindi cha takribani miaka 47. Katika kipindi hiki, limelipa gharama kubwa katika njia ya kudumisha uhuru na msimamo wake wa kusimama imara. Kwa hiyo, hatupaswi kuruhusu shinikizo za kiuchumi na propaganda za vyombo vya habari kusababisha kupuuzwa matakwa ya msingi ya taifa la Iran."

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu amesisitiza kuwa; matakwa yetu hayapaswi kubaki katika yale mambo saba yaliyotajwa katika makubaliano ya awali pekee, bali suala la Palestina na kurejeshwa ardhi zilizokaliwa kwa mabavu kwa wamiliki wake halisi pia linapaswa kuzingatiwa.

Ayatullah Araaki, akizungumzia uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa utawala wa Kizayuni, amesema: "Mpaka pale mikono ya utawala wa Kizayuni itakapozuiliwa kufanya uhalifu na uchokozi, haiwezekani kuzungumzia kupatikana uadilifu na kumalizika migogoro ya eneo hili; kwa sababu nchi za Ulaya na Marekani zimeshiriki katika uhalifu wa utawala huu."

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Elimu za Kidini ameendelea kusema kuwa; nchi hizo zimeungana na kushirikiana kwa kutoa silaha, rasilimali za kifedha, uungaji mkono wa kisiasa na msaada wa kijeshi, na kwa kufanya hivyo zimeweka mazingira ya kuendelezwa vitendo vya utawala wa Kizayuni. Hadi sasa, bado zinaendelea kutoa misaada na uungaji mkono wao.

Mlango-Bahari wa Hormuz unapaswa kugeuzwa kuwa nyenzo ya kutimiza matakwa ya Muqawama

Ayatullah Araaki, akizungumzia umuhimu wa Mlango-Bahari wa Hormuz katika mizani ya kiuchumi ya nchi za Magharibi, amesema: "Leo, Mlango-Bahari wa Hormuz umekuwa mojawapo ya maeneo muhimu zaidi ya kutegemea kiuchumi kwa Ulaya na Marekani. Kwa mtazamo huu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo muhimu wa kimkakati mikononi mwake. Kwa hiyo, uwezo huu unapaswa kuzingatiwa na kutumiwa mpaka matakwa ya Muqawama yatimizwe."

Akieleza kuwa matakwa ya Muqawama hayahusu suala la Palestina pekee, amesema: "Sisi tunaamini kwamba, kwa kuwa sasa uwezo na nguvu hii ya kimkakati iko mikononi mwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, masuala ya Palestina, Lebanon na Yemen pia yanapaswa kufuatiliwa katika mfumo wa matakwa ya Muqawama."

Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu ameongeza: "Haina mantiki kwamba kwa miaka mingi wananchi wa Palestina waendelee kukabiliwa na hali ya kukimbia makazi yao, mauaji makubwa na uhalifu usio na mwisho, na hali kama hiyo iendelee pia nchini Lebanon na Yemen, lakini mbele ya mazingira haya, tusitumie uwezo uliopo kufuatilia matakwa yetu na kumaliza migogoro hii."

Uamuzi wa mwisho kuhusu Mlango-Bahari wa Hormuz uko mikononi mwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mjumbe wa Baraza la Kutambua Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu, mwishoni mwa mazungumzo yake, amesisitiza kuwa mitazamo iliyotolewa kuhusu suala hili ni mapendekezo tu, akieleza: "Hata hivyo, uamuzi wa mwisho katika suala hili uko chini ya mamlaka ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Na chochote atakachoamua na kutangaza, sisi tunakichukulia kuwa ndio kauli ya mwisho isiyokuwa na nafasi ya kupingwa."

Ayatullah Araaki ameeleza kuwa; wao ni wafuasi wa mwongozo wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na watasalimu amri mbele ya uamuzi na mtazamo wake.

Ameongeza kuwa; maelezo haya ni mapendekezo tu ambayo huenda akayakubali au asiyakubali. Hata hivyo, kwa hali yoyote ile, jambo atakalolikubali na kuliamua ndilo litakalokuwa hoja ya kisheria ya Kiislamu kwao na msingi wa utekelezaji wao.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha